MISINGI YA MIFUKO YA UWEKEZAJI WA PAMOJA
Uwekezaji katika mifuko ya pamoja ni rahisi kuliko unavyofikiria. Ni njia nzuri ya kukuza mtaji kwa wale wenye malengo ya muda mfupi, kati na ya muda mrefu.
Mifuko hii ni aina ya uwekezaji wa pamoja ambayo inaruhusu wawekezaji walio na malengo sawa kuwekeza fedha zao kwa pamoja kwenye jalada la dhamana au mali zingine.
Wawekezaji (wenye vipande) hawamiliki dhamana hizo za mfuko moja kwa moja. Umiliki wa mfuko umegawanywa katika umiliki wa vipande. Kadiri mfuko unavyoongezeka au kupungua kwa thamani ndivyo thamani ya kipande huongezeka au kupungua ipasavyo. Idadi ya vipande inategemea bei ya ununuzi wa kipande,wakati wa uwekezaji na kiwango cha pesa kilichowekezwa.
Kawaida, faida ya uwekezaji kwa wamiliki wa vipande hupatikana kwa mfumo wa gawio la mapato na kukua kwa mtaji, inayotokana na uwekezaji wa pamoja. Kila kipande kinapata mapato sawa, yaliyotokana na kiwango kilichowekezwa kama mtaji katika kipindi chochote.
Uwekezaji katika mifuko ya uwekezaji wa pamoja, huhamisha utaalam wote wa uwekezaji kwa wale wenye uwezo wa kusimamia masuala ya uwekezaji na hao ndiyo sisi, UTT -AMIS (Wasimamizi wa Mfuko).
FAIDA
Kuna faida zingine kubwa ambazo mtu anaweza kupata kwa Kuwekeza katika mifuko inayosimamiwa na UTT AMIS.
UWEKEZAJI MSETO
Kutawanya uwekezaji hupunguza hatari ya uwekezaji na kuongeza mapato. Hakuna kikomo kwa idadi ya wawekezaji ambao wanaweza kumiliki vipande kwenye mfuko wetu wowote. Kuwepo kwa wawekezaji wengi zaidi katika mfuko ndivyo rasilimali zaidi na faida inavyopatikana kwa uwekezaji mseto katika mfuko.
WELEDI
UTT AMIS ndiyo wasimamizi wa mifuko yote sita. Ni wasimamizi wa viwango vya juu vya kimataifa wenye rekodi ya mapato mazuri katika soko hapa nchini. Ikumbukwe, wasimamizi bora wa mifuko husaidia kuongeza kipato cha mwekezaji.
USALAMA
Mifuko ya uwekezaji wa pamoja inaratibiwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na inadhibitiwa na sheria ya mifuko ya uwekezaji wa pamoja yenye lengo la kumlinda mwekezaji. Kanuni hizi zinahusiana na shughuli za kampuni za Usimamizi/Uwendeshaji wa mifuko ya uwekezaji wa pamoja.
UNAFUU
Mifuko ya uwekezaji wa pamoja inakupa unafuu wa kununua hisa za makampuni yanayofanya vizuri. Mwekezaji ana uwezo wa kupata hisa zote ambazo mfuko umewekeza kwa ununuzi mmoja.
URAHISI NA VIGEZO VYA UWEKEZAJI
Unaweza kuwekeza kwa muda mrefu au mfupi. Hakuna kipindi mahsusi/maalum cha uwekezaji kilichowekwa. Vipande vya mifuko ya uwekezaji wa pamoja ni rahisi kununua na ni rahisi kuuza. Mwekezaji anaweza kubadilisha mgawanyo wa mali kulingana na hali ilivyo mwekezaji anaweza kubadilisha uwekezaji kutoka uwekezaji wa msingi wa hisa (hisa) hadi dhamana ya mapato ya moja kwa moja (Hatifungani za muda mfupi na hati fungani za muda mrefu) au mchanganyiko wa aina yoyote utakohitajika. Hili linategemea na waraka wa toleo wa mfuko.
UKWASI
Mwekezaji anaweza kuwekeza kwa muda mrefu au mfupi kulingana na sifa za mfuko. Mwekezaji anauwezo wa kuamua wakati anaotaka kuuza vipande pia kupata pesa za mauzo ya vipande kwa muda mfupi. Kwa kuwa uwekezaji ni zoezi la muda mrefu, wawekezaji wanashauriwa kuwa na mtazamo wa muda mrefu ili kunufaika zaidi na uwekezaji.